Saturday, August 16, 2014

Mjadala mkali wabunge kuteuliwa kuwa mawaziri

Wajumbe wa bunge la katiba wakiwakwenye kikao Dodoma
SUALA la mawaziri kuwa wabunge au hapana, limezua mjadala mkali katika vikao vya kamati mbalimbali za Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea mjini hapa. Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Makamu Mwenyekiti wa Kamati Namba 10, Salmin Awadhi Salmin, alisema katika kamati yake mjadala kuhusu Rasimu ya Katiba ni mzuri na wajumbe wamekuwa wakitoa hoja mbalimbali za kuiboresha.
"Yapo mambo mengi yamejitokeza katika majadiliano ya ibara za sura mbalimbali tulizojadili kwa wiki hii, ambazo ni Sura ya 7,8, 11, 14 na 15, lakini mjadala mkubwa ulikuwa kwenye suala la mawaziri wawe wabunge au vipi.
Baraza jipya la mawaziri
"Kama mnavyojua Rasimu ya Tume ya Jaji Joseph Warioba imependekeza mawaziri wasitokane na wabunge ili kuweka mgawanyo mzuri wa madaraka," alisema Mwenyekiti huyo.
Alifafanua kuwa wajumbe wanaounga mkono ibara hiyo, licha ya suala la mgawanyo wa madaraka, lakini pia wanajenga hoja kuwa lazima mihimili hiyo ijitegemee kwa maana ya Bunge na Serikali.
"Wanasema mawaziri wakiwa wabunge kama ilivyo sasa, wakiwa kwenye vikao vya bunge wanatetea msimamo wa serikali zaidi, pia mgawanyo wa madaraka unakua haupo.
"Wanaotaka mawaziri waendelee kuwa wabunge, wanasema ukiwatoa nje ya Bunge inakuwa ngumu hasa unapotaka ufafanuzi wa mambo mbalimbali yanayofanywa na serikali, kwa vile waziri anaweza kupanga safari yoyote kwani hahusiki na Bunge," alisema Salmin.

No comments:

Post a Comment