Wakati kukiwa na malalamiko kwamba Bunge
la Maalumu la Katiba linagharimu fedha nyingi za walipakodi, uongozi wa
taasisi hiyo umetumia Sh142.56 milioni kukodi vipaza sauti kutoka Kituo
cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis
Hamad alithibitisha kukodiwa kwa vipaza sauti hivyo kwa ajili kamati
zote 12 na kwamba kila gharama ya chumba kimoja kwa siku ni Dola 450 za
Marekani (Dola moja ni wastani wa Sh1,650).
Kwa maana hiyo Bunge, hilo linatumia
Dola 5,400 sawa na Sh8.91 milioni kwa siku kugharimia vipaza sauti
katika vyumba 12 vinavyotumiwa na kamati hizo na kwa siku 16 ambazo
kamati zitakutana, gharama hizo zitafikia Sh142.56.
“Vifaa vya sauti tulivyokuwa navyo
vinalalamikiwa, vilikuwa siyo standard (viwango) hasa vya mazungumzo,
tumekodi kutoka Ukumbi wa Mikutano wa AICC na tumekuwa nao usiku mzima
kuvifunga,” alisema.
Alisema tangu wavifunge, hawajawahi
kupata malalamiko tena kutoka katika kamati kuhusu ubora na kwamba
gharama za kukodisha vifaa hivyo itatoka katika fungu la dharura la
Bunge Maalumu.
“Mara ya kwanza walituambia gharama zao
ni Dola 500 kwa siku lakini tukajadiliana nao, hivyo tukafikia kiwango
hicho cha Dola 450,” alisema.
Hamad alisema vifaa vya awali ambavyo
vililalamikiwa na wajumbe kuwa havitoshi, vinatoa sauti nje ya majengo
na kwa jinsi vilivyo, vinalazimika kutembezwa ukumbini, hivyo
kusababisha usumbufu.
Malalamiko ya gharama
Suala la gharama limekuwa likiibuka mara
kwa mara na wakati mwingine kutajwa kama sababu ya kuahirishwa kwa
Bunge hilo kwa kuwa hakuna uhakika wa kupatikana kwa akidi inayotakiwa
kufikia uamuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba
alilalamikia kile alichokiita “matumizi ya kufuru” ya Bunge Maalumu
wakati hakuna uhakika wa kupatikana kwa Katiba Mpya.
No comments:
Post a Comment