Dar/Dodoma. Rais Jakaya Kikwete amesema
suala la uraia wa nchi mbili linaonekana kutokuwa na nguvu kwa sasa
kutokana na kutojitokeza katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hivyo
kutoingia katika Rasimu ya Katiba inayojadiliwa sasa bungeni.
Kauli ya Rais Kikwete imekuja wakati
suala hilo likionekana kuwagawa wajumbe katika Kamati za Bunge Maalumu,
kutokana na kuwapo kwa mapendekezo kwamba suala uraia pacha liingizwe
kwenye rasimu hata kama halikuwekwa na Tume.
Juzi, suala hilo liliwagawa wajumbe wa
Kamati Namba mbili inayoongozwa na Waziri Kiongozi mstaafu wa Zanzibar,
Shamsi Vuai Nahodha na kusababisha ibara hiyo kukosa theluthi mbili ya
kura kutoka pande zote za muungano.
Akizungumza katika kongamano maalumu
linalowakutanisha Watanzania waishio nje ya nchi Dar es Salaam jana,
Rais Kikwete alisema suala hilo limekosa wasemaji wanaoguswa moja kwa
moja ambao wangeweza kulitetea, hivyo kutokuwa miongoni mwa vipaumbele
katika rasimu hiyo.
“Msijipe matumaini kwa sababu kwa namna
ilivyoandikwa kwenye Rasimu ya Katiba, haiwezi kuzaa uraia wa nchi
mbili, bali inaweza kutoa stahiki ya fursa wanazoweza kupata Watanzania
waishio nje ya nchi, kupitia sheria,” alisema.
Kongamano hilo la kwanza la siku mbili
linawakutanisha Watanzania waishio katika nchi 17 duniani,
lililoandaliwa na Asasi ya Tanzania Diaspora Initiative (TDI).
Rais Kikwete alisema Serikali yake
inafahamu umuhimu wa kupatikana kwa uraia pacha kwa watu wake lakini
suala la uraia ni la kikatiba na siyo la Rais kwa kuwa Katiba ndiyo
inayoamua.
Alisema hata chama chake (CCM),
kilipojaribu kuliingiza lilionekana kutokuwa na nguvu ya kutosha kwa
kuwa hakuna ambaye lilikuwa likimgusa moja kwa moja.
Aliwashauri kuwatumia wajumbe katika
Bunge linaloendelea mjini Dodoma ili wapaze sauti zao na ikiwezekana
watumie fursa zote za mawasiliano kufikisha ujumbe wao.
“Sisi upande wa Serikali tunaliona ni
suala jema, ila halina nguvu kwa sababu wabunge wengi haliwagusi moja
kwa moja, hivyo si rahisi kulipigania. Mbona nchi nyingine watu wao
wananufaika na hili! Kwa nini hapa kwetu lishindikane?” alihoji.
Ndani ya kamati
Habari kutoka ndani ya kamati zinasema
wajumbe wamegawanyika kuhusu suala hilo na wengine wameshindwa kufikia
mwafaka kama ilivyotokea katika Kamati namba 11 inayoongozwa na Mbunge
wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela.
Mwandishi wetu alidokezwa kuwa kulikuwa
na mvutano mkali kuhusu pendekezo la kuanzishwa kwa uraia pacha na hadi
sasa uamuzi wa kura bado haujafanyika kuhusu suala hilo na wajumbe wa
Kamati namba tano inayoongozwa na Hamad Rashid Mohamed walikubaliana kwa
kauli moja kuongeza ibara inayoruhusu kuanzishwa kwa uraia pacha.
Itakumbukwa kuwa suala hilo ndilo
lilizua mvutano mkali baina ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji
Frederick Werema na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsi na Watoto,
Sophia Simba kiasi cha kutoleana maneno makali wakati wakilijadili
kwenye Kamati namba 6 inayoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Uhusiano na Uratibu), Steven Wasira.
No comments:
Post a Comment