Friday, July 11, 2014

WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli amesisitiza Serikali haitaweka matuta ya vizuizi vya kupunguza ajali katika barabara zote zilizoko nchini.
Alisema hayo juzi katika Kijiji cha Igogo wilayani Igunga Mkoa wa Tabora, baada ya wananchi kulalamika juu ya ajali zinazotokea katika eneo lao kutokana na mwendo kasi wa magari.
Magufuli alisema, kwa sasa serikali haiwezi kuweka matuta katikati ya barabara kwani ikiweka matuta itakuwa imevunja Sheria za Usalama Barabarani Namba 32 ya mwaka 1973.
Alisema alama zitakazowekwa ni za pundamilia. Waziri huyo ambaye alionya juu ya vitendo vya wananchi, kung’oa alama zinazowekwa barabarani, alihimiza wazitunze.
Awali, zilisikika sauti kutoka kwa wananchi zikieleza furaha ya ujio wa Waziri Magufuli, huku wakimwomba wawekewe matuta katika eneo hilo, kutokana na ajali zinazotokea mara kwa mara.
“Ujio wako leo kwetu ni furaha kubwa kwa sisi wakazi wa kijiji cha Igogo, hivyo tunakuomba sana utuwekee matuta eneo hili kwani zaidi ya watu wanne wamepoteza maisha kwa kugongwa na gari,” alisikika mmoja wananchi hao.
Wakati huo huo, Waziri alitembelea daraja la mto wa Mbutu na kukagua ujenzi unaoendelea.
Pia, alizungumza na wananchi wa kata ya Mbutu katika eneo hilo la daraja, linalotarajia kukamilika mwezi ujao. Magufuli alisema serikali inatambua kudaiwa fedha na wakandarasi, wanaojenga barabara za lami sehemu mbalimbali nchini.
Alisema wakati jiwe la msingi la ujenzi wa lami lilipowekwa, wapo baadhi ya watu walisema haitajengwa Mkoa wa Tabora “Lakini kwa sasa wamejionea wenyewe kwa macho yao lami iliyojengwa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi,” alisema.
Hata hivyo, alisema gharama za ujenzi wa barabara ya lami mkoani Tabora ni zaidi ya Sh bilioni 500, ambazo hakuna fedha zilizotolewa na wafadhili, bali yote ni ya serikali.
Alisisitiza, serikali chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete ni tajiri, ikizingatiwa kwamba wakoloni waliacha kilometa 1,300 za barabara za lami, lakini, sasa serikali ya Kikwete imejenga kilometa 11,154 za lami na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tano Afrika, zinazotumia fedha zake za ndani.
Kuhusu madeni ya kampuni za ukandarasi mkoani Tabora, alisema ni Sh bilioni 111. Kati ya hizo, kampuni sita za China zinadai Sh bilioni 105 huku kampuni za Tanzania zikidai Sh bilioni sita.
Kwa upande wa nchi nzima, Magufuli alisema serikali inadaiwa zaidi ya Sh bilioni 600. Hata aliwahakikishia wakandarasi watalipwa fedha zote.
 

No comments:

Post a Comment