Wakati jamii ikiwa bado haijasahau
mateso aliyoyapata mtoto Nasra Mvungi na kusababisha kifo chake, tukio
lingine la aina hiyo limetokea katika Kijiji cha Matongola, Tarafa ya
Magole Wilaya ya Kilosa, baada ya kubainika mtoto wa miaka sita akiwa
amefichwa uvunguni mwa kitanda na kufanyiwa vitendo vya kikatili na mama
yake mzazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,
Leonald Paulo alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa taarifa za
mateso ya mtoto huyo zilifikishwa Kituo cha Polisi wilayani Kilosa saa
za mchana jana, baada ya uongozi wa kijiji na kata kutoa taarifa na
tayari mwanamke huyo amekamatwa kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Mama aliyefanya ukatili huo anafahamika
kwa jina la Sala Mazengo ambaye alimficha ndani mtoto wake aliyefahamika
kwa jina la Devota Malole na kumfanyia vitendo vya kikatili ikiwa
pamoja na kutompa chakula, wala kumfanyia usafi.
Baada ya kufichuliwa kutoka alipofichwa,
mtoto huyo alionekana kuwa dhaifu kiafya kutokana na kukosa lishe
pamoja na mazingira aliyokuwa akiishi kutoridhisha, jambo ambalo ni kosa
kisheria, pia ukiukwaji wa haki za watoto.
Inadaiwa kuwa tangu mwaka 2009 Sala
amekuwa akimficha mtoto wake huyo ambaye sasa amelazwa katika Hospitali
ya Wilaya ya Kilosa kwa ajili ya kupatiwa vipimo na matibabu.
Hata hivyo, mwanamke huyo alipoulizwa
alidai kuwa afya ya mtoto wake ilikuwa mbaya tangu alipozaliwa kutokana
na magonjwa ya mara kwa mara, pia hali ngumu ya maisha ilichangia
kudhoofisha afya ya mtoto huyo.
Alidai kuwa ana watoto sita, pia alikiri
kumlaza chini mtoto huyo kutokana na kuwa na kitanda kimoja, ambacho
hakiwatoshi watoto hao.
Aliongeza kuwa hata chakula amekuwa akikipata kwa shida kutokana na kushindwa kufanya kazi kwa kuwa ana mtoto mwingine mdogo.
Kamanda Paulo alisema kuwa mwili wa
mtoto huyo umedhoofu kutokana na kufichwa ndani kwa muda mrefu na bado
mwanamke huyo hajaeleza sababu za kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya
mtoto huyo.
“Siwezi kutoa taarifa ya kidaktari,
lakini kutokana na afya ya mtoto yule na mazingira tuliyomkuta ni
dhahiri alikuwa akipata mateso na kufanyiwa vitendo vya ukatili. Hata
hivyo, uchunguzi zaidi tunaufanya na kwamba taratibu za kumfikisha
mtuhumiwa huyo Kituo Kikuu cha Polisi mkoani hapa zinaendelea,” alisema
Kamanda Paulo.
Alisema kuwa mpaka sasa bado
haijafahamika kama mtoto Davota ni mlemavu au la na kwamba taarifa za
afya ya mtoto huyo zitatolewa baada ya madaktari kumfanyia uchunguzi wa
kina.
No comments:
Post a Comment