Tuesday, July 22, 2014

MAKALA; Teknolojia Jinsi waongoza ndege wanavyopatikana

Wiki iliyopita Mkufunzi Mwandamizi wa usimamizi wa ndege kutoka Chuo cha Mafunzo ya Usafiri wa Anga (CATC), Shadrack Kalinga alifafanua namna ndege inavyoongozwa kuanzia kupaa mpaka kutua katika kiwanja kingine.
Leo atafafanua jinsi mchakato wa kuwapata waongoza ndege na mafunzo wanayopitia mpaka kufuzu kuifanya kazi hiyo.
Kama zilivyo kada nyingine za sayansi, waongoza ndege wanapitia mafunzo ya kina ya nadharia na vitendo katika vyuo vya usafiri wa anga.
“Kwa kawaida mafunzo ya uongozaji ndege huchukua wiki 20: kumi ni mafunzo ya nadharia na 10 nyingine katika vitendo kupitia mashine maalumu (simulators).
“Hata hivyo, hapa nchini mara nyingi wiki hizo huwa zinazidi kwa sababu kuna miezi mitatu katikati ya kwenda kwenye mafunzo ya vitendo katika viwanja vikuu vya ndege nchini,” anasema Kalinga.
Kuhusu kiwango cha ufaulu kinachotakiwa, Mkuu wa Chuo hicho Margareth Kyarwenda anasema unahitajika ufaulu wa hali ya juu wa mosomo ya sayansi na hesabu.
“Ili uweze kusoma kozi za usafiri wa anga unatakiwa uwe umafaulu vizuri sana masomo sayansi na hesabu hali kadhalika Kiingereza na Jiografia kidato cha nne na cha sita. Pia kama umemaliza shahada basi uwe umesoma masomo ya uhandisi na kufaulu vizuri,” anaeleza Kyarwenda.
Anabainisha kuwa mwanafunzi anapoanza masomo hayo huanza upya na shahada yake ya awali haichukuliwi kama mwendelezo wa masomo--uzamili au Stashahada.
Mashine maalumu za kufundishia uongozaji ndege
Katika kujifunza uongozaji ndege, wanafunzi wanahitaji wapitie nadharia pamoja na vitendo.
Katika vitendo hupewa mazoezi namna ya kuziongoza ndege kupitia mitambo ya ‘simulator’ yenye uwezo wa kutengeneza hali za hewa za namna mbalimbali.
Mitambo hii inajumuisha mfumo wa skrini zilizofungwa kwa kubananishwa kwa muundo wa duara ili kutoa muono endelevu kutoka ya kwanza hadi ya mwisho. Mfumo huo wa duara hupimwa kwa kipimo cha nyuzi kati ya 280 au zozote ndani ya 360.
Mitambo huongozwa na mfumo wa kompyuta (operating system) na kuunganishwa mashine za kuongezea ambazo huwekwa kutokana na idadi watu wanaohitajika katika chumba husika.
Mwanafunzi aliyepo kwenye zamu ya mafunzo hayo hukaa katikati na wengine kumsaidia kwenye mitambo mingine ya mbele.
“Humu ndani kuna programu ambazo zinaweza kutengeneza uwanja wa ndege. ghushi wa mahali popote ulimwenguni na pia kuweka hali za hewa kama mawingu, mvua, jua kali, ukungu na mengine mengi,” anasema Kalinga.
Kwa mujibu wa Kyarwenda mtambo mpya waliofunga katika chuo hicho cha CATC kinachomilikiwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) unagharimu takriban Sh1.5 bilioni na ni wa kisasa zaidi.
Kalinga pia naongeza kuwa chumba cha ‘simulator’ katika chuo chao kinabeba wanafunzi wanane na kila mmoja anatakiwa afanye mafunzo kwa vitendo kwa jumla ya saa nane—saa moja kila siku.
Anabainisha baada ya kumaliza mafunzo hayo mwanafunzi huyo anaenda kufanya tena mazoezi kwa vitendo miezi mitatu kwa kuongoza ndege moja kwa moja.
“Baada ya hapo wanamfanyia tathmini na akifaulu anapelekwa katika bodi ya uamuzi ya (TCAA) ambapo anafanyiwa usaili kwa mahojiano.
“Ukipita hapo sasa ndiyo unapewa leseni na kwenda kuanza kuongoza ndege huku ukisimamiwa,” anasema Kalinga.
Mkufunzi huyo anasema baada ya kuangaliwa kwa muda, mwanafunzi huyo anajaza ‘log book’ ambayo itamfanya awe amehitimu na kuanza kazi kama mwongozaji.

No comments:

Post a Comment