Friday, November 28, 2014

Mahakama yamtakasa Sheikh Issa Ponda

Sheikh Issa Ponda akiwa mahamani akisikiliza mashitaka yanayo mkabili
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemtakasa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda dhidi ya hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyomtia hatiani katika kesi ya jinai iliyotokana na mgogoro wa ardhi wa Chang’ombe Markazi.

Sheikh Issa Ponda akitoka mahama ya hakim mkazi kisutu akiwa chini ya ulizi mkali wa makachero
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Agustine Shangwa baada ya kuridhika na hoja za rufani za Sheikh Ponda kupitia kwa Wakili wake, Juma Nassoro kupinga hukumu na hatia ya Mahakama ya Kisutu.

Mbali na kumfutia hatia hiyo, pia Jaji Shangwa alimshauri Sheikh Ponda kufungua kesi ya madai dhidi ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), pamoja na Kampuni ya Agritanza Ltd iliyonunua eneo la Chang’ombe Markazi.
Ponda alikata rufani mahakamani hapo akipinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyomtia hatiani katika kesi ya jinai namba 245 ya mwaka 2012, iliyokuwa ikimkabili yeye na wenzake 49.
Katika rufaa hiyo, Sheikh Ponda kupitia kwa wakili wake, Nassoro aliwasilisha jumla ya hoja sita za kupinga hukumu hiyo.
Hoja hizo zilikuwa ni pamoja na ya kudai kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilikosea kumtia hatiani kwa kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani kwa kosa hilo la kuingia kwa nguvu katika eneo hilo la mgogoro.

No comments:

Post a Comment